MAJINA YA WALIOPATA MIKOPO YATANGAZWA

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itatangaza orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi walioomba na kupangiwa mikopo Alhamisi, Oktoba 17 mwaka huu.
Hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa maombi ya mikopo yapatayo 55,444 ya wanafunzi ambao wamepata udahili katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es salaam leo (Jumatatu, Oktoba 14, 2019), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema wanafunzi watakaopangiwa mikopo wataweza kupata taarifa zao kupitia akaunti zao kwenye mtandao wa taasisi hiyo.
Pamoja na kutangaza orodha hiyo, Badru amesema HESLB pia imeamua kutoa fursa kwa waombaji 4,794 ambao bado hadi sasa hawajakamilisha maombi yao kukamilisha kwa kuambatisha nyaraka muhimu mtandaoni.
Kuhusu malengo ya mwaka huu wa masomo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB amesema Serikali imetenga TZS 450 bilioni ambazo zitawanufaisha jumla ya wanafunzi 128,285.
Kati yao, wanafunzi zaidi ya 45,000 watakuwa ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo. Bajeti ya mwaka wa masomo 2018/2019 ilikuwa TZS 427.5 bilioni na iliwanufaisha jumla ya wanafunzi 123,329

Post a Comment

0 Comments